Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jaji Hatem al-Na’san, mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi katika matukio ya Sweida (kusini mwa Syria), ametangaza kuwa watu waliokuwa wakionekana kwenye video katika mitandao ya kijamii wakifanya makosa walikamatwa na kupelekwa kwenye wizara za ulinzi na mambo ya ndani.
Akiashiria kwamba uchunguzi wa kamati hiyo haupendelei mtu yeyote na hauko chini ya amri wala mwongozo wa afisa yeyote wa serikali, alibainisha kuwa Kamati ya Uchunguzi katika matukio ya Sweida inafanya kazi kulingana na viwango vya Umoja wa Mataifa.
Kauli za Jaji Hatem al-Na’san zilitolewa katika mkutano wa waandishi wa habari huko Damascus, ambapo Kamati ya Uchunguzi ya matukio ya Sweida iliwasilisha taarifa ya maendeleo ya kazi yake, ikasisitiza uhuru wake, na kuomba kuongezewa muda wa shughuli zake.
Al-Na’san alisema: “Yale yaliyotokea mwezi Julai 2025 katika mkoa huu wa Sweida — mauaji, ubakaji, uharibifu, uhamishaji wa kulazimishwa na pia kuenea kwa hotuba za chuki — ni ‘ukiukaji mkubwa’ ambao hauwezi kushughulikiwa kwa suluhisho la juujuu au kisiasa, bali unahitaji uchunguzi madhubuti unaozingatia matakwa ya kisheria.”
Akaongeza kuwa kamati katika kazi yake inarejea uamuzi uliotolewa na Waziri wa Sheria mwaka 2025, mfumo wa kisheria uliobainishwa katika kifungu cha 51 cha Tamko la Katiba, pamoja na mikataba na makubaliano ya kimataifa ambayo Syria imeridhia na ambayo ni sehemu ya sheria ya kitaifa.
Alifafanua kuwa mamlaka ya kamati inajumuisha kuchunguza jinai na makosa kwa mujibu wa sheria ya adhabu ya Syria namba 148 ya mwaka 1949, na pia kanuni za sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, ikiwemo mikataba minne ya Geneva na kifungu cha tatu cha pamoja, kwa kuzingatia misingi ya kibinadamu, kutobagua, ulazima na uwiano.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mbinu iliyochukuliwa na kamati inaendana na kanuni za Umoja wa Mataifa kuhusu Kamati za Uchunguzi, na inajumuisha kugundua upeo wa matukio, kupokea malalamiko, kubaini utambulisho wa waliohusika, kubainisha uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja, kuhakikisha kutokuwepo kwa kinga dhidi ya adhabu, na kutoa mapendekezo ya kuzuia kurudiwa kwa makosa hayo.
Al-Na’san aliendelea kusema kuwa mtazamo wa kamati unategemea kanuni ya kutodhuru, na kuhakikisha ulinzi kwa mashahidi, waathiriwa, familia zao, na wafanyakazi wa kamati. Pia alisisitiza kuwa kazi ya kamati iko katika mwelekeo wa kusaidia mchakato wa kuimarisha maridhiano ya kitaifa kati ya pande zinazopingana.
Alibainisha kuwa wajumbe wa kamati wanafanya kazi kwa uhuru kamili bila kupokea maelekezo ya aina yoyote kutoka upande wowote, na wameshikamana na kutokuwa na upendeleo kwenye uchunguzi wa makosa yote yanayodaiwa kufanywa na pande zote, huku wakiheshimu usiri wa taarifa na mazungumzo.
Al-Na’san alisema: “Kamati inajitahidi kupata imani kwa waathiriwa, mashahidi na wengine ili kushirikiana na kuwapa taarifa, na kamati haitoi ahadi zisizowezekana kutimizwa, bali inaweka mipaka halisi ya matarajio ya familia za waathiriwa juu ya uwezo wa kamati.”
Akaeleza kuwa timu za uchunguzi katika miezi mitatu iliyopita zimefanya ziara za moja kwa moja katika maeneo waliyokeuka kwenye vitongoji vya Damascus, Idlib, Sweida na Daraa na pia katika hospitali, na zimekusanya na kuhifadhi vielelezo kwa njia inayohakikisha uhalali wake mbele ya mahakama; pamoja na kubaini mifumo ya mashambulizi na njia za ukiukaji na kuzifafanua kisheria.
Akaongeza kuwa kamati imefanya mahojiano na manusura, waathiriwa na mashahidi wa moja kwa moja, na imefuatilia mafaili ya waliokamatwa, waliotekwa na waliopotea, na katika baadhi ya kesi kumekuwa na maendeleo.
Inapaswa kusemwa kuwa; mwezi Julai 2025, mkoa wa Sweida kusini mwa Syria ulishuhudia mapigano makali yaliyosababisha kuuawa na kujeruhiwa kwa makumi ya watu, uhamishwaji wa lazima, na ukiukwaji mkubwa, na serikali ya Syria ikaunda Kamati ya Kitaifa ya Uchunguzi kwa ajili ya kufichua ukweli na kuwawajibisha wahalifu.
Matukio hayo — ambayo yalizuka kati ya vikosi vinavyohusishwa na wizara za ulinzi na mambo ya ndani za serikali ya Syria na makundi ya kikabila kwa upande mmoja, na makundi ya wazawa wa Druze kwa upande mwingine — yalizua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mvutano wa kimadhehebu katika eneo nyeti lenye idadi kubwa ya wa Druze, na yakasababisha kuwepo kwa ushirikiano wa kimataifa uliomalizika kwa usitishaji mapigano.
Matukio hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 50, kujeruhiwa mamia ya watu, na kuhamishwa maelfu, pamoja na mauaji katika Hospitali ya Taifa ya Sweida. Matukio haya yalielezewa kuwa “mauaji ya kimadhehebu yenye umwagaji damu”, huku kukiwa na ripoti za mauaji ya kiholela na utekaji nyara kutoka pande zote mbili.
Athari hizi zilisababisha makubaliano manne ya usitishaji mapigano na mkutano wa pande tatu nchini Jordan mwezi Agosti 2025 kwa ushiriki wa Syria, Jordan na Marekani ili kudhibiti mgogoro huo.
Maoni yako